TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Arusha
imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 74.8 zilizolipwa kwa watumishi na
semina hewa. Aidha watumishi wa umma wamesisitizwa kufanya kazi kwa
maslahi ya umma, kwa kuzingatia suala zima la uadilifu na kuacha
kuwashawishi wananchi kutoa fedha ili wapate huduma.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha, Frida Wikessy wakati
alipotoa taarifa ya utendaji kazi wa tasisi hiyo katika kipindi cha
Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu.
Wikessy alisema fedha hizo zimerejeshwa serikalini baada ya kuziokoa
kutokana na watumishi hewa pamoja na semina hewa zilizoandikwa kwa
kughushi saini ili watu wajipatie fedha. Alisema fedha hizo zilitokana
na watumishi hewa Idara ya afya na elimu ambapo kulikuwa na watumishi
wameacha kazi, kufa na wengine kuhama vituo vya kazi, lakini serikali
iliendelea kulipa.
Aidha katika kipindi hicho mkoa huo ulipokea jumla ya malalamiko 248
kwa njia mbalimbali na kati ya hayo majalada 24 ya uchunguzi
yanaendelea, yapo katika hatua mbalimbali. Frida alisema katika uongozi
wa awamu ya tano umekuwa na ongezeko la wananchi kutoa taarifa nyingi
tofauti na miaka ya nyuma, hali inayosababisha kupokea malalamiko yalio
sahihi na yasio sahihi. Pia alisema katika kipindi hicho mashauri 14
yalisikilizwa na kati ya hayo 10 yalishinda katika kesi za jinsi na
uhujumu uchumi